Je
twaelewa mfumo wa uongozi ulivyo katika kila taasisi nchini mwetu na je twajua
chanzo cha kuwepo matabaka mbalimbali? Katika makala haya nimeangazia na
kuyajibu maswali haya paruwanja kama yavyodhihika uongozini
Kenya
imegawika katika matabaka walalahai na hawa ni walio na uwezo wa kukimu
mahitaji yao ya kila siku na wenye uwezo wa kuishi maisha ambayo kila mja
angependa au anatamani kuyaishi. Kundi la pili ni la walalahoi ambalo ndilo
hasa linajumuisha asilimia kubwa zaidi nchini. Hili kukithi mahitaji yao ni
kero kubwa sisemi ni ngumu. Hili ni kundi ambalo linapigania kile ambacho
kilisalia baada ya kundi la awali kukinai. Hili ni dhahiri utembeapo katika
sehemu za madongoporomoka pale hali ya maisha ni ya kubahatisha chambilecho
wenyeji.
Kuna
matabaka mengine mawili ambayo kwa kiasi kikubwa huchangia kuwepo kwa matabaka
ya hapo awali. Kuna la watawala na
watawaliwa ama ukipata muda sema wapiga kura na wapigiwa kura. Haya mawili kwa
maoni yangu ndiyo huamua hatma ya nchi yoyote ile. Kwanza kabisa wapiga kura
ndio mhimili mkuu wa kudhibiti nchi. Nina uhakika kwamba baada ya makala haya
msomaji na mpenzi na mkubali wa uhalisia atakubaliana nami. Wakati wa kampeini
za kisiasa ndio kila hila ya kila aina huzinduliwa. Kila anayesimama jukwaani
kutoa hotuba hudai kwamba atageuza sehemu au kitengo alichochaguliwa kuhudumu
au kuwakilisha kuwa paradiso. Sisi tukiwa wapiga kura hushangilia na kuwapa
sifa bila hata kujua kuwa ni chui kavalia ngozi ya kondoo chambilecho wazee
wetu. Wanapoingia madarakani huzuka na sera madhubuti ambazo kwangu ni za
kuwafumba wananchi wapiga kura macho. Pindi tu baada ya kutulia ofisini inakuwa
ni mwamba ngoma huvuta upande wake. Unakuwa ni wakati wa kuvuvia viriba na
kujenga makasri yote kwa hisani ya mali ya mpiga kura. Baada ya miaka mitano
wanarudi hata bila zaibaki za usoni na kuomba kura nasi bila kufikiria tunawapa
kura na kuwarejesha mamlakani. Tabia ya imeridhishwa tangu hapo jadi na
waliotangulia.
Taswira hii ya uongozi na siasa si tofauti na
vyuoni au uchaguzi na siasa katika vyuo vikuu. Imekuwa ni kawaida kuandaa
midahalo ili kubaini ambacho viongozi wetu watatufanyia baada ya kutwaa
uongozi.katika midahalo hii ubabe na matapo hushamiri kila mmoja akijaribu
kumpiku mpinzani wake. Hapa sauti na jinsi utashughulikia maswala yaliyoulizwa
ndio nguzo muhimu ya kushawishi wafuasi. Kinachokerekete maini ni kwamba mtindo
ule ule wa maji hufuata mkondo huendelezwa. Tunaahidiwa paradise kumbe matokeo
ni jehanamu chambilecho Muingereza. Unagundua waliochaguliwa wanawakilisha watu
tofauti kabisa na waliowachagua na inakuwa kwanza ni kushulikia maswala
yanayohusisha maisha yangu. Matokeo ya hayo ni kuwa na usimamizi kandamizi na
minongono ya kila aina kwa ajili ya uongozi. Hii huathiri utendakazi wa chuo husika
kwani ushirikiano haupo.
Nitakuwa
mtovu wa taadhima nisipowashukuru na kuwapa mkono wa heko wanaoelewa
kilichowapeleka ofisini. Hili ndilo kundi ambalo kwao masilahi ya watawaliwa
hupewa kipaumbele. Ni jambo la kuajabia kwamba adinasi hawa ni adimu kama
maziwa ya kuku ama kama tone jangwani.
Ili
kupata nchi na chuo tunachotamani ni kwetu sisi watawaliwa kuketi na kujaribu
kutafakari mustakabali wetu kuhusiana na viongozi ambao tunapanga kuchagua.
Aidha nisionekane mwanaharakati au mwanamapinduzi bali ninachotaka kusema ni
kwamba tuzitathmini sera ambazo viongozi wetu wanatuahidi na utekelezwaji wazo
na tusiwe na dhana ya kisiasa na kikabila tunapopiga kura.
Kwa
viongozi wetu nawapiga mijeledi kwa kuwasaliti wafadhili wao na kukosa kuwawajibikia.
Mwandishi: Samwel Mburu
No comments:
Post a Comment