Mimi kama kiumbe niliyebahatika kuzaliwa katika
sayari hii, nimemeamua kukupa kongole ewe Malkia Kiswahili kwa sababu wewe ni
shujaa. Licha ya madhila yote tumewahi kukufanyia sisi kama waja hapa duniani,
wewe umekuwa mkarimu kwa kutufanyia fadhila nyingi ambazo sisi binadam
hatukustahili machoni pako. Kwa hilo, pokea shukran sufufu kutoka kwangu kwa niamba ya wapenzi
wako wote duniani.
Naomba niguzie zile njia umeonyesha ukakamavu na
ushujaa wa hali ya juu kwa kustahimili mawimbi makali na tufani zinazotokea
katika bahari hii ya maisha. Wengi wamejaribu kwa udi na uvumba kukunyang`anya
kizazi cha bala lako afrika. Mahali ambapo wewe ulizaliwa na ukafaham kuwa
nyumbani. Niliona wakikunyanganya hata watoto wadogo kwe shule ya chekechekea. Niliona wakipokea
mijeledi mikali kwa sababu ya kukuhusudu na kukuenzi, lakini ulifika na
kuwafariji kwa mishororo ya kuliwaza nyoyo zao zilizo umia. Na kwa wale
hawakukufa moyo, nawaona mahali uliwafikisha ewe Kiswahili.
Wengine wamepokea hadhi kubwa sana duniani.
Sina haja ya kuwataja majina kwa sababu unawajua bayana ila niseme hao ni wanao kindakindaki. Wapo
wale wakereketwa wa kukutaftia mahali pako katika jamii. Bila kumsahau Yule mwanao Usadh Wala bin Wala. Si unajua
mpaka ameanzisha Chuo cha Wasta?
Chuo ambacho kinaeneza kila mbinu muhimu ya
kukupatia wana wengi wa afrika na jirani zake.
Nimeona ukiwashukuru wanao na wapenzi kindakindaki. Mimi
kwanza ulifanya nikaja chuo kikuu sasa nami ni mwana mlimani! Wengine umewatunuku
nafasi ya kupaa juu angani mpaka ng`ambo ya maji. Wengine uliwapa ajira na
ukawapa shukran sufufu kwa kuinua kipato chao.
Hongera kwa kustahimili mawindo ya wale wanao
kuwinda ili wakuangamize. Hawa ni wale wanaowadharau wanao wanaokuenzi
kindakindaki wakisema wanaozungumza Kiswahili wana hadhi ya chini. Wengine wamo
mbioni kueneza kasumba kwamba Kiswahili ni kigumu, Vipi na tangu lini mwana wa
mji akaita mgeni Baba? Ama kweli wamewachanganya baadhi ya wanao. Licha ya hayo
nimekuona ukiwatuma wajumbe wako kukutetea katika mijadala yetu na hata ya
kimataifa. Kwa kweli wewe ni mwerevu hakika.
Nimeona kiamboni wengine wamekuja na lugha zingine
ili wakutoe katika ramani ya dunia. Wameleta sheng` ili wakunyang`anye
hadhira kwa wana wa miji na vijiji. Jambo moja limenishangaza, ni jinsi ambavyo
wewe unaendelea kusambaa kote duniani. Nimewaona wanao wakipeleka ujumbe wako
mbali na nyumbani ugaibuni. Marekani, China, Ulaya wote wako mbioni kusoma
sheria na kaida zako ili wawe na nafasi katika karne hii ya utandawazi. Nimekuona
umepenya mpaka ndani ya technologia. Nina furaha kwa sababu niliyaona makao
yako kwenye mtandao. Bila shaka hutakufa kipenzi changu Kiswahili. Sasa kamusi
nyingi nimeziona zinazokuangazia wewe, na hata katika katiba ya Kenya wewe
ulijioatia nafasi yako madhubiti katika dola hili.
Afrika yote inakukumbatia tena kwa hamu. Kuna jambo
ambalo nimeliona ukilifanya lakini bado halijatimia. Sio lazima niwe nabii
lakini ninauwezo wa kusema hivi karibuni utakuwa wa kutumika Afrika nzima. Nimewaona
wakitafuta lugha moja ya kuwaunganisha
wana Afrika na alama zako ziko kidedea kuliko lugha za Fulani, Yoruba, Mande na Hausa ambazo zilipigiwa
kura kujitoza ulingoni kukabiliana nawe. Lakini linalo nipa tabasamu, ni kwamba
wewe bado uko mbali na wenzio kwa sababu ya historia yako ndefu na machapisho
kadha wa kadha. Pili usuli wako ni wa kibantu na lugha nyingi Afrika ni za
kibantu na ndio maana ikilinganishwa na wenzako, wewe una wasemaji wengi. Ndio maana
wasomi kama Wole Soyinka, Mohammed Hasan Abdulaziz na wengine walipokutana mjini Lagos Mwaka wa 1976, walikupigia kura na hakika hiyo siku itafika kipenzi changu
na utafikwa koja.
Ombi langu kuu kwako ni kwamba endelea kuzidi
kung`ang`ana na hatimaye utafanikiwa. Ndio najua una shida kidogo kidogo kama
za misamiati mingi tu ya kueleza mambo mengi ya kisayanzi na kiteknologia
lakini usife moyo kwani wenzako pia wamekopa. Hata wewe una uhuru wa kukopa.
Licha ya hayo watie wanao shime ili wasichoke katika utafiti kila siku na
kuleta misamiati kwa sababu wewe unakua kwa njia moja kubwa sana.
Nakuomba uzidi kuwakumbusha wale wanao eneza dhana
potovu kwamba wewe ni wa haiba ya chini ukiwapa mifano ya wanao wengi ambao
wameendelea sana kimaisha kupitia kukukumbatia
wewe. Nangoja kuona siku ile utatumika kama nembo ya kutambulisha Afrika
na dunia kwa jumla. Hakika hongera kipenzi changu kwa juhudi kubwa ulizonazo kwa kuwafaidi
wanadam na njia mufidi ya kuwasiliana. Mungu azidi kuwabariki wana na wapenzi
wako duniani.
Mwandishi: Franklin Momanyi. Mwanafunzi Chuo Kikuu cha Chuka.
Mwandishi: Franklin Momanyi. Mwanafunzi Chuo Kikuu cha Chuka.
No comments:
Post a Comment