Monday 24 November 2014

MAENDELEO YA KISWAHILI KATIKA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO (TEHAMA)

Teknolojia ya habari na mawasiliano imekuwa kiungo muhimu sana katika maendeleo ya watu duniani. Wamekuwa wakitumia teknolojia hii katika kufanya mawasiliano muhimu, kufanya biashara na mambo mengine mengi yanayowanufaisha watu. Tarakilishi ni mojawapo ya kifaa kilicholeta mapinduzi katika TEHAMA kama asemavyo Katambi (2011) “Kompyuta ama Tarakilishi katika lugha ya Kiswahili ni kifaa ambacho kimebadilisha kabisa mfumo wa maisha ya binadamu katika miongo takribani sita iliyopita. Kutokana na kuwapo kifaa hiki dunia imejikuta katika maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi chochote kile katika historia ya kuwapo kwake. Kifaa hiki kimeleta mabadiliko makubwa sana katika maisha ya kawaida ya binadamu. Kifaa hiki kimesababisha mambo mengi kufanyika katika hali ambayo hakika isingewezekana au ambayo awali ingeonekana kama ya kufikirika. Kompyuta imeyafanya maisha kuwa rahisi zaidi. Kompyuta imeifanya dunia kuwa Kama kijiji kidogo ambacho unaweza kukizunguka katika muda mfupi Sana wa sekunde chache”. Maneno haya ya Katambi yanaonesha ni jinsi gani kompyuta ilivyo muhimi katika TEHAMA, mawasiliano yote ya teknolojia ya habari hufanywa kwa kutumia kompyuta, mfano; matangazo ya redio na televisheni, magazeti na n.k huandaliwa kwa kutumia kompyuta na kuwa tayari kwa ajili ya kupasha habari. TEHAMA ina umuhimu kama ulivyoangaziwa hapa: Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa ujumla imechangia sehemu kubwa kuleta maendeleo hasa katika kipindi hiki cha karne ya 21 ambapo utandawazi umeenea ulimwengu mzima na kuifanya dunia kuwa kama kijiji ambapo watu huwasiliana na kufanya kazi na biashara kwa pamoja kama wapo katika kijiji kimoja, mambo haya yote yanafanikiwa kwa kuwezeshwa na TEHAMA. Kama asemavyo Kamau (2009) kuwa ushirikiano wa kimataifa katika mambo kama vile siasa, biashara, uchumi , michezo n.k huwezeshwa na kurahisishwa na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ambayo imeuunganisha ulimwengu mzima kimawasiliano. Kwa maelezo haya tunaweza kuona ni jinsi gani TEHAMA ilivyo kuwa muhimu katika ulimwengu wa sasa. Lugha ni muhimu sana katika suala zima la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hatuwezi kuhamisha maarifa yaliyopo katika teknolojia hii bila kutumia lugha na kwa hiyo ili kuwapo na maendeleo endelevu kupitia TEHAMA ni lazima pia lugha inayotumika kuhamisha maarifa ya teknolojia hii iwe inaleweka kwa watumiaji husika. Hii itakuwa rahisi kwao kuilewa na kuitumia teknolojia hii vilivyo kwa sababu lugha inayotumika ni lugha wanayoifahamu na ni lugha yao. Kama tujuavyo bara la Afrika halijaendelea sana kwa kiwango cha kuzalisha teknolojia zitakazo kubalika katika masoko ya kimataifa kama yafanyavyo mabara mengine hususani mabara ya Ulaya na Marekani, kwa hiyo kulingana na hali hii Afrika imekuwa ikiingiza teknolojia za kigeni kutoka Mabara mengine hasa Marekani na Ulaya, teknolojia hizi zimekuwa zikiingizwa kwa lugha za kigeni jambo ambalo hufanya watumiaji wengi wa Waafrika kushindwa kumudu matumizi ya teknolojia hizi kwa sababu hawajui lugha iliyotumiwa. Kila jitihada zinazofanywa katika kufikia malengo fulani huwa hakukosi changamoto. Katika jitihada za kufanya Kiswahili kuwa lugha ya kiteknolojia kumetokea changamoto nyingi, moja wapo iliyo kuu kabisa ni kwamba lugha ya Kiswahili haimilikiwi na taifa lolote tajiri kwa hiyo katika harakatika za kuendeleza inakumbana na changamoto nyingi kama vile ukosefu wa fedha na hata utayari wa viongozi wa kisiasa kukiendeleza Kiswahili ni mdogo sana, hata hivyo harakati hizi zinapingwa na mataifa ambayo lugha zao zimeendelea sana kiteknolojia kwa kuhofia kwamba zitafunikwa na matumizi ya Kiswahili. Wapo tayari kutoa misaada ili kuendeleza lugha zao kukididimiza Kiswahili kitu ambacho kinafanya harakati za kukiendeleza Kiswahili kuwa ngumu kwani nchi kinamozungumzwa Kiswahili hazina pesa za kupambana na mataifa makubwa yanayopigia upatu lugha zao. Kutokana na sababu hizo, kasi ya uundaji wa istilahi za kiteknolojia imekuwa ndogo sana, kwani kufanya hivyo pia kunahitaji pesa, na mara nyingi pesa zimekuwa zikitolewa na wahisani au makampuni yanayohusika kitu kinachotokea mara moja baada ya muda mrefu sana. Pia, viongozi wa serikali hawajatilia mkazo suala hili, hawajaona umuhimu wa kukiendeleza Kiswahili kitenolojia. Nguvu zao nyingi wameziweka katika miradi mingine ya kimaendeleo huku wakisahau kabisa kuwa Kiswahili pia kinahitaji kwenda sambamba na maendeleo hayo. Kwa hiyo hii imekuwa ni changamoto katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili. Kwa kuwa istilahi hizi zimekuwa zikifanywa na watu tofautitofauti, ni muhimu kuwapo na jopo maalumu la kusanifisha istilahi hizi kabla hazijasamabazwa. Kwa kufanya hivi hakutakuwa na matumizi tofauti ya istilahi katika dhana moja. Hali hii inajitokeza sana endapo uundaji wa istilahi utakuwa umefanywa katika makundi tofauti. Utayari wa watumiaji; watumiaji wengi kutumia programu za tarakilishi kwa lugha za Kiswahili. Madai yao ni kwamba istilahi za Kiswahili ni ngumu sana na hivyo si rahisi kuzitumia, kwa mfano, wengi wamezoea kusema install na kwa hiyo ukiwaambia kwamba install kwa Kiswahili twasema sanidi watabaki wakikushangaa na wataona kama unawapa kazi kubwa sana. Kwa hivyo hii nayo inasababisha matumizi ya Kiswahili katika vifaa vya kiteknolojia hususani kompyuta kuwa hafifu. Samwel Mburu samwelmburu@yahoo.com