Sunday 14 December 2014

CHANGAMOTO ZIKUMBAZO WALIMU KATIKA UFUNDISHAJI




Ni bayana kama mchana kwamba ufundishaji wa lugha ya Kiswahili una changamoto si haba. Mtoto azaliwapo huwa hajijui hajitambui. Mawasiliano yake na watu walio karibu huwa ni kupitia kwa kilio ambacho kwa wengi hukera masikio na kuwafanya wakeshe usiku kucha wakijaribu kumnyamazisha yule mwana. Lakini hakuna refu lisilo na ncha kwani kilio hiki hakidumu milele. Huwa ni cha wakati tu.
    
 Mtoto hujiunga na shule na kumpata mwandani mwingine kwa jina mwalimu. Hapa mtoto huona mapya na kuanza kuyaiga kama kasuku. Mdarisi naye hujitahidi ima fa ima ili kumwelekeza mwanagenzi wake kwa njia iliyo bora zaidi. Hapa ndipo changamoto huanza kujitokeza kwa mwalimu na kwa mwanafunzi. Mwanafunzi mwenyewe huwa ashaiga lugha hafifu ya pale nyumbani kwao kwa hivyo mwalimu huona ugumu kumfundisha lugha sanifu. Ngeli huwa ni mwamba usioweza kutikisika. Utamsikia mwanafunzi huyu wa chekechea akisema ," vitabu zake, viatu zangu, nywele yangu " na kadhalika. Matatizo haya hasa hutokana na lugha uchwarauchwara izungumzwayo nyumbani. Vilevile husababishwa na athari ya lugha ya mama.
    
 Afikapo katika darasa la nne , huanza uandishi wa insha. Ikiwa mwalimu wa chekechea na madarasa ya chini hakuweka msingi imara kwa mwanafunzi huyu , basi uandishi wa insha hapa huwa janga kubwa. Mwalimu wa darasa hili la nne hana budi kujifunga masombo ili ajaribu kurekebisha makosa mengi yafanywayo na mwanagenzi katika kiwango hiki. Msingi wake unaoyumbayumba wafaa kufanywa imara katika kiwango hiki. Ni kazi ngumu sana kwa mwalimu kumkosoa mwanafunzi kila wasaa lakini lisilo budi hutendwa. Kiwango hiki ndicho humpanua mwanafunzi mawazo akaweza kuandika visa mbalimbali kwa ufasaha. Ni vyema mwalimu ampe mwanafunzi mada anazoweza kuizifahamu na kuzieleza. Pia mwalimu ajaribu sana asije akawatisha wanafunzi na visa vya vifo na mauaji. Ni vyema kumwezesha mtoto afurahie uandishi wake. Kumbuka , ili mwanafunzi apasi katika somo lolote lile lazima alipende na kulifurahia. Walimu tujaribu kuwapa wanafunzi wetu mada kulingana na umri wao.
    
 Kutokana na msingi imara alioupata katika madarasa ya chini , mwanafunzi huyu hatakuwa  na matatizo mengi katika darasa la nane. Lakini hapa napo mwalimu hukumbwa na misukumo kutoka pande zote . Mwanafunzi huyu lazima apasi katika mtihani wa kitaifa! Msukumo huu pia humsumbua mwanagenzi akawa kama zumbukuku. Wote wawili ,mwalimu na mwanafunzi, huanza kutafuta matopa na matopa ya mabuku ambayo mengi huwakanganya zaidi. Ni vyema tuelewe kuwa uandishi mzuri si ule wenye maneno makubwa makubwa bali unaoeleweka na ulioandikwa kwa lugha sanifu. Mwanafunzi asaidiwe kuchagua mapambo ya lugha yafaayo ili asipapie mapambo yoyote yale. Walimu nasi tusisitize ufuataji wa maudhui na upatanisho ufaao wa sarufi. Tusiwatese wanafunzi na maneno mazito na misemo ya kujibunia. Tufuate silabasi kikamilifu ili wanafunzi wawe tayari kuufanya mtihani ifaavyo. Mwana akifundishwa vyema katika shule ya msingi huwa bora katika shule za sekondari.
   
Changamoto ni nyingi kwetu walimu lakini kazi hii lazima tuifanye. Ni jukumu letu kuweka msingi imara wa taifa letu na kuitetea lugha ya Kiswahili.
         
Mwalimu DAUDI MAINA  
  KERUGOYA KAUNTI YA KIRINYAGA