Ni bayana kama mchana kwamba
ufundishaji wa lugha ya Kiswahili una changamoto si haba. Mtoto azaliwapo huwa
hajijui hajitambui. Mawasiliano yake na watu walio karibu huwa ni kupitia kwa
kilio ambacho kwa wengi hukera masikio na kuwafanya wakeshe usiku kucha
wakijaribu kumnyamazisha yule mwana. Lakini hakuna refu lisilo na ncha
kwani kilio hiki hakidumu milele. Huwa ni cha wakati tu.
Mtoto hujiunga na shule na kumpata mwandani
mwingine kwa jina mwalimu. Hapa mtoto huona mapya na kuanza kuyaiga kama
kasuku. Mdarisi naye hujitahidi ima fa ima ili kumwelekeza mwanagenzi wake kwa
njia iliyo bora zaidi. Hapa ndipo changamoto huanza kujitokeza kwa mwalimu na
kwa mwanafunzi. Mwanafunzi mwenyewe huwa ashaiga lugha hafifu ya pale nyumbani
kwao kwa hivyo mwalimu huona ugumu kumfundisha lugha sanifu. Ngeli huwa ni
mwamba usioweza kutikisika. Utamsikia mwanafunzi huyu wa chekechea akisema
," vitabu zake, viatu zangu, nywele yangu " na kadhalika. Matatizo
haya hasa hutokana na lugha uchwarauchwara izungumzwayo nyumbani. Vilevile
husababishwa na athari ya lugha ya mama.
Afikapo katika darasa la nne , huanza uandishi
wa insha. Ikiwa mwalimu wa chekechea na madarasa ya chini hakuweka msingi imara
kwa mwanafunzi huyu , basi uandishi wa insha hapa huwa janga kubwa. Mwalimu wa
darasa hili la nne hana budi kujifunga masombo ili ajaribu kurekebisha makosa
mengi yafanywayo na mwanagenzi katika kiwango hiki. Msingi wake unaoyumbayumba
wafaa kufanywa imara katika kiwango hiki. Ni kazi ngumu sana kwa mwalimu
kumkosoa mwanafunzi kila wasaa lakini lisilo budi hutendwa. Kiwango hiki ndicho
humpanua mwanafunzi mawazo akaweza kuandika visa mbalimbali kwa ufasaha. Ni
vyema mwalimu ampe mwanafunzi mada anazoweza kuizifahamu na kuzieleza. Pia
mwalimu ajaribu sana asije akawatisha wanafunzi na visa vya vifo na mauaji. Ni
vyema kumwezesha mtoto afurahie uandishi wake. Kumbuka , ili mwanafunzi apasi
katika somo lolote lile lazima alipende na kulifurahia. Walimu tujaribu kuwapa
wanafunzi wetu mada kulingana na umri wao.
Kutokana na msingi imara alioupata katika
madarasa ya chini , mwanafunzi huyu hatakuwa na matatizo mengi katika
darasa la nane. Lakini hapa napo mwalimu hukumbwa na misukumo kutoka pande zote
. Mwanafunzi huyu lazima apasi katika mtihani wa kitaifa! Msukumo huu pia
humsumbua mwanagenzi akawa kama zumbukuku. Wote wawili ,mwalimu na mwanafunzi,
huanza kutafuta matopa na matopa ya mabuku ambayo mengi huwakanganya zaidi. Ni
vyema tuelewe kuwa uandishi mzuri si ule wenye maneno makubwa makubwa bali
unaoeleweka na ulioandikwa kwa lugha sanifu. Mwanafunzi asaidiwe kuchagua
mapambo ya lugha yafaayo ili asipapie mapambo yoyote yale. Walimu nasi
tusisitize ufuataji wa maudhui na upatanisho ufaao wa sarufi. Tusiwatese wanafunzi
na maneno mazito na misemo ya kujibunia. Tufuate silabasi kikamilifu ili
wanafunzi wawe tayari kuufanya mtihani ifaavyo. Mwana akifundishwa vyema katika
shule ya msingi huwa bora katika shule za sekondari.
Changamoto ni nyingi kwetu walimu
lakini kazi hii lazima tuifanye. Ni jukumu letu kuweka msingi imara wa taifa
letu na kuitetea lugha ya Kiswahili.
Mwalimu DAUDI MAINA
KERUGOYA KAUNTI YA
KIRINYAGA