Wakati wa ukoloni mwafrika hakuruhusiwa
kumiliki kitu chochote ambacho kilidhaniwa kuleta mapato. Hali hii iliendelea hadi
pale uhuru ulipatikana ndiposa umilisi wa kitu kwa upande wa mwafrika ukawa.
Mtu alipopapata kazi ofisini ilikuwa ni fahari kubwa sana na alitarajia
kuheshimika sana. Pindi baada ya uhuru nchi nyingi zilijitawala ikiwemo nchi
yetu na wakati huo nafasi za kazi serikalini na hata makampuni ya kibinafsi
zikawa nyingi kutokana na utengenezaji wa bidhaa muhimu. Watu walifurahia hali
ya maisha kwani kila mja aliweza kuyakidhi mahitaji yake. Faida nyingi naweza
nikazitaja hadi nibakie kuandika riwaya.
Hiyo ni historia wala haiwezi ikajiradidi.
Kutokana na kero la ufisadi nafasi za
kazi zimewa finyu kwani asiye na kitu cha kupeana au kutokuwa na nasaba na
wakubwa hapati kazi. Hali hii imesababisha hali ya maisha kuwa ghali mno. Fauka
ya hayo imepelekea baadhi ya makampuni na taasisi za uundaji kupata hasara
kutokana na kuwaajili watu ambao hawajahitima ambao wakiulizwa hawaungami.
Utasikia vijana wengi ambao wamehitimu masomoni wengi wao wakiwa wa vyuo vikuu
wakilia hamna. Hao ndio utawaona wakati wote wakipiga gumzo zisizo na manufaa
yoyote maishani. Haya hamna yeyote anayepinga wala kukataa kuwa hakuna kazi. Jambo
hili li wazi kama meno ya ngiri chambilecho watangulizi wetu.. swali langu ni
je iwapo ulipitia shule ya msingi, upili na hatimaye chuo kikuu ni nini ambacho
huwezi ukafanya ili kujipa riziki? Tatizo letu kubwa limewa kutegemea tu kazi
ya ofisi hasa wale ambao wamehitimu vyema masomoni. Uzembe na ukosefu wa kuwa
wabunifu kumezidi kuharibu hali ya maisha.
Ni jambo la busara na mwafaka sana kuwa na
maono ila kuna dhana potovu ambayo walohitimu au wanaopania kuhitimu kuwa
pasipo kufanya kazi ofisini kazi nyingine zozote si kazi. Kwa kweli
tumezungukwa na nafasi nyingi tu za kazi ila tu hatutaki kuzitumia kwa hofu ya
kusemwa kuwa walihitimu ila hawafanyi kazi ya viwango vyao. Tusione kana kwamba
waliosema kuwa waja ni ngamba hawakosi la kuamba walikosea. Waache wawe
vidudumtu na waeneza umbeya lakini mwisho wa siku watalala. Ufaulu ama usifaulu
lazima binadamu ataongea hivyo tusiogope kusemwa kwa chochote tukifanyacho. Upo
wakati ambao tutahitajika kufanya mambo yaliyo chini ya viwango vyetu ili
kukidhi mahitaji yetu wala tusione haya ama aibu kuyachangamkia. Ukweli na
ukweli uchi uliopo ni kwamba nafasi za ajira ni finyu sana hivyo twafaa
kujitengenezea nafasi za kazi. Utagundua kuwa mamantilie wengi wamehitimu ila
hawaogopi kusemwa kwa kazi wafanyazo.
Nawarai wanaohitimu kuwa tusitegemee
kuajiriwa ila tupanie kubuni nafasi za kazi.ili kukimu mahitaji yetu ya kila
siku. Tutupilie mbali dhana ya kwamba lazima tuajiriwe. Nchi nyingi ambazo
zimeendelea imekuwa ni juhudi kutoka kwa wanaanchi za kujituma na kuelewa kuwa
maisha ni yao hivyo kutegemea kuajiriwa itakuwa ni kama kualika taabu na
matatizo kwako.
Nikihitimisha nasema kwamba kazi ni kazi na
mchagua jembe si mkulima kwamba mtegemea cha nduguye hufa maskini aidha
changu hata kiwe kibovu ni bora kuliko chetu. Tutumie maarifa tuliyopata
maishani kujipa ajira.
Kauli yangu ni kuwa, Katu sitachagua wala
kubagua kazi yoyote mradi tu yanipa riziki.
Mwandishi: Samwel Mburu
No comments:
Post a Comment