Ni jambo la kuudhi sana kumwona mtu akidondokwa na
machozi kwa kuachwa na mpenzi wake miezi michache tu baada ya kuanzisha
uhusiano. Wengi hulia, hupoteza mwelekeo huku wengine wakijitia kitanzi baada ya
tukio hili kutokea. Naomba tulitathmini
swala hili kwa kifupi. Iwapo mpenzi wako amefariki, je, utaishi maisha ya ukapera
milele? Iwapo umegundua kwamba mpenzi
wako si mwaminifu kwako, utahisi vipi? Mnapokuwa katika uhusiano wa mbali, yepi
huibuka?
Asilimia kubwa ya walio kwenye uhusiano wowote wa
kimapenzi, hutafuta mpenzi mwingine pindi tu mwenzi wao dhati wanapoelekea
jongomeo. Wengi hudai kuwa ni njia ya kuponya vidonda huku idadi ama asilimia
ndogo wakibaki kapera. Na wanapogundua kuwa wapenzi wao si waaminifu kwao na
kuwa wanajihuzisha na ‘mpango wa kando’ hujitia kwenye uwanja na kutafuta
mipango yao ya kando, bila kujali madhara kama, magonjwa ya zinaa huenea kuingia
kwenye familia.
Wengi kati ya wale ambao wako na uhusiano wa mbali hufeli kwani wapenzi hukosa wakati tosha
wa kuwa pamoja ili kusemezana na kujuliana hali. Hufika wakati ambapo kidosho
hataki mwanamume na kwa sababu mpenzi wake yuko mbali humlazimu kutafuta wa
karibu ambaye watakuwa wakionana mara nyingi. Ni wachache ambao huweza
kusimamisha uhusiano wa mbali hasa walio na uwezo wa kutembeleana mara nyingi
kwani hili huchangia sana katika kukuza uhusiano.
Ni bayana kuwa ‘Upendo haudumu’ kwani mtu huweza
kumsahau mpenzi wake na kumchukua mwingine na hili laweza jirudia mara kwa
mara. Sioni sababu mwafaka ya kusema umempenda mtu kwani kila siku, kila dakika
binadamu hupendezwa na anachokiona.‘Upendo au undani ni jambo la kuwaza na sioni haja
ya kulia unapoachwa na mpenzio. Ninaloliamini ni kuwa hakuna ‘mapenzi’. Hayo ni
madai ya kiakili tu. Huwezi pendezwa na mwingine iwapo unampenda uliye naye.
Mwandishi: BENSON WAWERU, Chuo Kikuu cha Chuka
No comments:
Post a Comment