Monday, 24 November 2014
MAENDELEO YA KISWAHILI KATIKA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO (TEHAMA)
Teknolojia ya habari na mawasiliano imekuwa kiungo muhimu sana katika maendeleo ya watu duniani. Wamekuwa wakitumia teknolojia hii katika kufanya mawasiliano muhimu, kufanya biashara na mambo mengine mengi yanayowanufaisha watu. Tarakilishi ni mojawapo ya kifaa kilicholeta mapinduzi katika TEHAMA kama asemavyo Katambi (2011) “Kompyuta ama Tarakilishi katika lugha ya Kiswahili ni kifaa ambacho kimebadilisha kabisa mfumo wa maisha ya binadamu katika miongo takribani sita iliyopita. Kutokana na kuwapo kifaa hiki dunia imejikuta katika maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi chochote kile katika historia ya kuwapo kwake. Kifaa hiki kimeleta mabadiliko makubwa sana katika maisha ya kawaida ya binadamu. Kifaa hiki kimesababisha mambo mengi kufanyika katika hali ambayo hakika isingewezekana au ambayo awali ingeonekana kama ya kufikirika. Kompyuta imeyafanya maisha kuwa rahisi zaidi.
Kompyuta imeifanya dunia kuwa Kama kijiji kidogo ambacho unaweza kukizunguka katika muda mfupi Sana wa sekunde chache”. Maneno haya ya Katambi yanaonesha ni jinsi gani kompyuta ilivyo muhimi katika TEHAMA, mawasiliano yote ya teknolojia ya habari hufanywa kwa kutumia kompyuta, mfano; matangazo ya redio na televisheni, magazeti na n.k huandaliwa kwa kutumia kompyuta na kuwa tayari kwa ajili ya kupasha habari. TEHAMA ina umuhimu kama ulivyoangaziwa hapa:
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa ujumla imechangia sehemu kubwa kuleta maendeleo hasa katika kipindi hiki cha karne ya 21 ambapo utandawazi umeenea ulimwengu mzima na kuifanya dunia kuwa kama kijiji ambapo watu huwasiliana na kufanya kazi na biashara kwa pamoja kama wapo katika kijiji kimoja, mambo haya yote yanafanikiwa kwa kuwezeshwa na TEHAMA. Kama asemavyo Kamau (2009) kuwa ushirikiano wa kimataifa katika mambo kama vile siasa, biashara, uchumi , michezo n.k huwezeshwa na kurahisishwa na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ambayo imeuunganisha ulimwengu mzima kimawasiliano. Kwa maelezo haya tunaweza kuona ni jinsi gani TEHAMA ilivyo kuwa muhimu katika ulimwengu wa sasa.
Lugha ni muhimu sana katika suala zima la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hatuwezi kuhamisha maarifa yaliyopo katika teknolojia hii bila kutumia lugha na kwa hiyo ili kuwapo na maendeleo endelevu kupitia TEHAMA ni lazima pia lugha inayotumika kuhamisha maarifa ya teknolojia hii iwe inaleweka kwa watumiaji husika. Hii itakuwa rahisi kwao kuilewa na kuitumia teknolojia hii vilivyo kwa sababu lugha inayotumika ni lugha wanayoifahamu na ni lugha yao. Kama tujuavyo bara la Afrika halijaendelea sana kwa kiwango cha kuzalisha teknolojia zitakazo kubalika katika masoko ya kimataifa kama yafanyavyo mabara mengine hususani mabara ya Ulaya na Marekani, kwa hiyo kulingana na hali hii Afrika imekuwa ikiingiza teknolojia za kigeni kutoka Mabara mengine hasa Marekani na Ulaya, teknolojia hizi zimekuwa zikiingizwa kwa lugha za kigeni jambo ambalo hufanya watumiaji wengi wa Waafrika kushindwa kumudu matumizi ya teknolojia hizi kwa sababu hawajui lugha iliyotumiwa.
Kila jitihada zinazofanywa katika kufikia malengo fulani huwa hakukosi changamoto. Katika jitihada za kufanya Kiswahili kuwa lugha ya kiteknolojia kumetokea changamoto nyingi, moja wapo iliyo kuu kabisa ni kwamba lugha ya Kiswahili haimilikiwi na taifa lolote tajiri kwa hiyo katika harakatika za kuendeleza inakumbana na changamoto nyingi kama vile ukosefu wa fedha na hata utayari wa viongozi wa kisiasa kukiendeleza Kiswahili ni mdogo sana, hata hivyo harakati hizi zinapingwa na mataifa ambayo lugha zao zimeendelea sana kiteknolojia kwa kuhofia kwamba zitafunikwa na matumizi ya Kiswahili. Wapo tayari kutoa misaada ili kuendeleza lugha zao kukididimiza Kiswahili kitu ambacho kinafanya harakati za kukiendeleza Kiswahili kuwa ngumu kwani nchi kinamozungumzwa Kiswahili hazina pesa za kupambana na mataifa makubwa yanayopigia upatu lugha zao.
Kutokana na sababu hizo, kasi ya uundaji wa istilahi za kiteknolojia imekuwa ndogo sana, kwani kufanya hivyo pia kunahitaji pesa, na mara nyingi pesa zimekuwa zikitolewa na wahisani au makampuni yanayohusika kitu kinachotokea mara moja baada ya muda mrefu sana. Pia, viongozi wa serikali hawajatilia mkazo suala hili, hawajaona umuhimu wa kukiendeleza Kiswahili kitenolojia. Nguvu zao nyingi wameziweka katika miradi mingine ya kimaendeleo huku wakisahau kabisa kuwa Kiswahili pia kinahitaji kwenda sambamba na maendeleo hayo. Kwa hiyo hii imekuwa ni changamoto katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Kwa kuwa istilahi hizi zimekuwa zikifanywa na watu tofautitofauti, ni muhimu kuwapo na jopo maalumu la kusanifisha istilahi hizi kabla hazijasamabazwa. Kwa kufanya hivi hakutakuwa na matumizi tofauti ya istilahi katika dhana moja. Hali hii inajitokeza sana endapo uundaji wa istilahi utakuwa umefanywa katika makundi tofauti. Utayari wa watumiaji; watumiaji wengi kutumia programu za tarakilishi kwa lugha za Kiswahili. Madai yao ni kwamba istilahi za Kiswahili ni ngumu sana na hivyo si rahisi kuzitumia, kwa mfano, wengi wamezoea kusema install na kwa hiyo ukiwaambia kwamba install kwa Kiswahili twasema sanidi watabaki wakikushangaa na wataona kama unawapa kazi kubwa sana. Kwa hivyo hii nayo inasababisha matumizi ya Kiswahili katika vifaa vya kiteknolojia hususani kompyuta kuwa hafifu.
Samwel Mburu
samwelmburu@yahoo.com
Thursday, 30 October 2014
Wazazi wapata afueni
![]() |
| Wanafunzi wa shule ya uoili wakiwa kwenye mahabara. |
Mapendekezo yaliyotolewa na jopo la
kutathmini karo za shule za upili ni mwafaka iwapo yataidhinishwa. Mapendekezo
hayo ya kupunguza karo kwa wanafunzi wa shule za upili za umma yanafaa na ni
afueni kwa wazazi ambao kidogo wamekuwa wakitwika mzigo mkubwa sana wa kulipa
kitita kikubwa cha fedha kila mwaka.
Tume hiyo inayoongozwa na aliyekuwa wazili
wa elimu Dkt Kilemi Mwiria ambaye sasa ni mshauri wa rais kuhusu maswala ya
elimu iliwasilishe ripoti yenye mapendekezo hayo kwa rais ambaye aliyapokea kwa
mwelekeo chanya na kusema kuwa kila motto anapaswa kupata elimu ya kimsingi.
Aidha rais aliongeza kusema kuwa serikali kuu itashirikiana na idara nyingine
pamoja na washikadau husika kuhakikisha kuwa hili litatimia.
Hatua hii itahakikisha kuwa visa vya
wanafunzi kuacha shule kwa ajili ya ukosefu wa karo imezimwa hivyo kwa
wanafunzi ambao huzembea katika masomo yao na kuacha shule hawatawa na sababu
ya kuacha hivyo basi waweza wakachukuliwa hatua za kisheria. Hii pia itatoa
nafasi sawa kwa kila mwanafunzi kupata elimu. Ni matumaini ya kila mzazi kuwa
Rais ataidhinisha mapendekezo hayo baada ya mashauriano na washikadau wote
katika sekta ya elimu.
Mwandishi ni Mburu Samwel
(Chuo Kikuu cha Chuka.)
Tuesday, 28 October 2014
JANGA KUBWA VYUONI
Wanafunzi wengi hupata furaha
wanapopata fursa ya kujiunga na chuo kikuu. Kwa mfano, nilipopata barua
yangu mwaka wa pili baada ya kuhitimu masomo ya kidato cha nne. Ilikuwa furaha,
shangwe, na nderemo kijijini mwetu kwa kuwa mwana wao alikuwa anajiunga na chuo
kikuu. Chuoni ni mahali ambapo mja akiingia akitoka atatoka akiwa mtu wa
thamani sana katika taifa lake. Ndo maana wote wanafuzu vyuoni huwa nguvu
kazi ya taifa na wanatumiwa kuendeleza uchumi wa dola. Lakini sasa, hiyo sifa imeanza
kufifia na kudidimia. Kwa nini?
Kitambo kidogo, wanafunzi
waliofuzu kwenda chuo kikuu walikuwa wanakaa nje ya chuo kikuu kwa mwaka mmoja
na nusu ivi kabla ya kuingia chuoni. Lakini kutoka mwaka wa 2011, wakati
Naibu wa Rais, Bw. William Ruto alipokuwa Waziri wa Elimu ya Juu,
wanafunzi wamekuwa wakijiunga na vyuo moia kwa moja.
Jambo nzuri lakini kulingana na
wakati huu, naona yapo maafa mengi yanakumba vyuo vikuu. Hawa wanafunzi
wanapata shida ya kudhibiti mhemko na kutoamini kwamba apo vyuoni. Mahali
ambapo pana uhuru wasio kadiria. Uhuru mkubwa kiasi kwamba hamna sare za
kuvalia, kila mmoja ana hiari ya kuvalia gwanda analoliona lamfaa. Ndiposa sasa
tunavyo zungumza, ukipitapita vibarabara vya chuo chochote kile mfano ukiwa
chuo cha Chuka, utatamaushwa na mavazi utakayo yaona. Juzi mzazi mmoja alizirai
alipomwona mwanaye amevalia jinsi hakuwa ametarajia kawe.
Shida nyingine ni ulevi wa pombe na
mihadarati. Kwa miaka nimekwa chuoni mwaka wanne sasa, mwaka huu mambo yamekuwa
makali kuliko miaka yaote. Wanafunzi haswa wa kike wanabugia mvinyo hadharani
bila kujali yeyote wala kuogopa sheria kali za chuo! Zinawafanya mpaka kupigana
kisha kuvunja sheria za chuo. Linalonishangaza ni kwamba hawana habari kwamba hapa
hakuna kutumwa mzazi nymbani! Ole wao kwa sababu wengi wako mbioni kuonana na
jopo la kushughulika nidhamu. Kwani yeyote ambaye amewahi kufika mbelel yake,
adhabu ni kubwa na wengi wao kuivumilia ni shida kwa sababu haistahimiliki
maishani mwao. Lakini lisilo budi hubidi na ukiyavulia nguo lazima uyakoge
ishara ya kukubali adhabu.
Nimeshuhudia mimi wanafunzi
wakipatatna asubuhi mchana wameoana na jioni wanafukuzana kisha kesi naletewa
mimi. Ngono kiholelaholela, na kutofwatilia ule mpangilio uliowekwa ili
kuendesha maisha chuoni. Hili limekuwa likiwapa tumbo joto viongozi wa
wanafunzi vyuoni nikiwa mmoja wao. Haswa idara yangu ikiwa ni ya kushughulikia
maslahi ya wanafunzi chuoni.
Badala ya kusoma, wapo mtandaoni
wakitumia mtandao kuwasiliana, katika mitandao ya kijamii. Maadam tovuti za
ngono zimefungwa, hawangebanduka mle. Mtihani ukifika, baadhi yao wanandika
mpaka ukuta almradi wapite kwa kuwa wakianguka hamna jingine ila kwenda
nyumbani. Ndo sababu ya kufanya lolote kuokoa maisha yake chuoni.
Nimeona uongozi umejaribu kuweka
mikakati ya kukabiliana na haya lakini bado maji yamezidi unga. Ninawaona
washauri nasaha wakiwa mbioni lakini mbio zao ni za sakafuni ambazo mpaka sasa
zinaishia ukingoni. Makundi ya madhehebu mbalimbli mbalimbali chuoni yakijaribu
kuleta msaada. Bado sijaoni dalili ya matumaini lakini lipo tumaini.
Kulingana nami, kuwa katika nafasi
ya kurudisha hadhi ya chuo kikuu, lazima warudishe ule mfumo wa kitambo. Kuokoa
malemgo ya chuo kikuu kisimama imara, sharti serikali irudishe ule mfumo wa
kitambo ili hawa wanafunzi wapate kuona maisha kudogo kabla ya kujiunga na chuo
kwa sababu hilo litafawafanya kubadili msimamo wao kuhusu maisha na kutia
bidii. Na pia kukomaa kidogo.
Pili nimeletewa kesi nyingi sana za
wanafunzi ambao hawana pesa za kuwafanya wawe chuoni. Nikiangalia wale wengi
wanakuja katika hali ya uchochole kwa sababu ya msingi wa familia labda. Lakini
ukiangazia vizuri, huyu mwanafunzi angekubaliwa kukaa nje kwa miaka miwili kama
ilivyokuwa zamani, angetengeneza hela kidogo za kumsaidia kusukuma maisha.
Akifika chuoni, ni kuamsha balaa na belua. Hata kukidhi mahitaji yake ni shida.
Karo nayo ni mlima unaowapa kiwewe kuukwea.
Kwa sasa inabidi ukumbuke
kwamba ile taasisi ya kupoeana mikopo kwa wanafunzi wa vyuo (HELB) pia
haina hela za kutosha kukidhi mahitaji ya wanafunzi wengi wanaongezeka
kila kukicha. Pia taasisi hiyo haina lingine ila kutekeleza amri ya selikali ya
kusema iwape wanavunzi wa vyu anuai mikopo. Usisahau kwamba taasis hiyo pia ina
jukumu la kuwapa mikopo wale wanafunzi wanaosomea ugaibuni. Kinaya ni kwamba
bado hawajaongezewa fedha kutoka hazina kuu ya kitaifa. Ndio maana
tutaendelea kuona migomo ya wanafunzi wa vyuo wakilalamikia ukosefu wa pesa.
Fauka ya hayo, mgaala muue na haki
mpe. Si wanafunzi wote ni watovu wa nidhamu. Wapo wenye maadili. Ukiwaangalia
vizuri unaweza sema wana malezi ya pende mbili. Hao hufanya kile
walinachostahili kufanya na hao ndio hutia for a katika Nyanja mbalimbali ya
kimasomo na hata spoti. Na hao ndiyo kila mtu na hata selikali inajivunia.
Ninapokamilisha ni vizuri kuuliza
swali? Je ni nani anayestahili kulaumiwa ka kupungua nidhamu katika vyuo
vyetu?
Mwandishi ni Frankline Momanyi, Mwanafunzi Chuo Kikkuu cha Chuka.
Tangazo....
Iwapo wewe ni mpenzi wa Kiswahili na una uwezo wa kuandika
makala kuhusu jambo lolote katika lugha sanifu ya Kiswahili basi unaweza jiunga
na waandishi wengine mashuhuri wanaoandikia FAHAMONLINE(www.fahamonline.blogspot.com ). Ukiandika
makala yako yatume kwa franklinpendo@gmail.com
Fanya hima ili usije ukabaki nyumba.
Friday, 24 October 2014
Hongera kiswahili.
Mimi kama kiumbe niliyebahatika kuzaliwa katika
sayari hii, nimemeamua kukupa kongole ewe Malkia Kiswahili kwa sababu wewe ni
shujaa. Licha ya madhila yote tumewahi kukufanyia sisi kama waja hapa duniani,
wewe umekuwa mkarimu kwa kutufanyia fadhila nyingi ambazo sisi binadam
hatukustahili machoni pako. Kwa hilo, pokea shukran sufufu kutoka kwangu kwa niamba ya wapenzi
wako wote duniani.
Naomba niguzie zile njia umeonyesha ukakamavu na
ushujaa wa hali ya juu kwa kustahimili mawimbi makali na tufani zinazotokea
katika bahari hii ya maisha. Wengi wamejaribu kwa udi na uvumba kukunyang`anya
kizazi cha bala lako afrika. Mahali ambapo wewe ulizaliwa na ukafaham kuwa
nyumbani. Niliona wakikunyanganya hata watoto wadogo kwe shule ya chekechekea. Niliona wakipokea
mijeledi mikali kwa sababu ya kukuhusudu na kukuenzi, lakini ulifika na
kuwafariji kwa mishororo ya kuliwaza nyoyo zao zilizo umia. Na kwa wale
hawakukufa moyo, nawaona mahali uliwafikisha ewe Kiswahili.
Wengine wamepokea hadhi kubwa sana duniani.
Sina haja ya kuwataja majina kwa sababu unawajua bayana ila niseme hao ni wanao kindakindaki. Wapo
wale wakereketwa wa kukutaftia mahali pako katika jamii. Bila kumsahau Yule mwanao Usadh Wala bin Wala. Si unajua
mpaka ameanzisha Chuo cha Wasta?
Chuo ambacho kinaeneza kila mbinu muhimu ya
kukupatia wana wengi wa afrika na jirani zake.
Nimeona ukiwashukuru wanao na wapenzi kindakindaki. Mimi
kwanza ulifanya nikaja chuo kikuu sasa nami ni mwana mlimani! Wengine umewatunuku
nafasi ya kupaa juu angani mpaka ng`ambo ya maji. Wengine uliwapa ajira na
ukawapa shukran sufufu kwa kuinua kipato chao.
Hongera kwa kustahimili mawindo ya wale wanao
kuwinda ili wakuangamize. Hawa ni wale wanaowadharau wanao wanaokuenzi
kindakindaki wakisema wanaozungumza Kiswahili wana hadhi ya chini. Wengine wamo
mbioni kueneza kasumba kwamba Kiswahili ni kigumu, Vipi na tangu lini mwana wa
mji akaita mgeni Baba? Ama kweli wamewachanganya baadhi ya wanao. Licha ya hayo
nimekuona ukiwatuma wajumbe wako kukutetea katika mijadala yetu na hata ya
kimataifa. Kwa kweli wewe ni mwerevu hakika.
Nimeona kiamboni wengine wamekuja na lugha zingine
ili wakutoe katika ramani ya dunia. Wameleta sheng` ili wakunyang`anye
hadhira kwa wana wa miji na vijiji. Jambo moja limenishangaza, ni jinsi ambavyo
wewe unaendelea kusambaa kote duniani. Nimewaona wanao wakipeleka ujumbe wako
mbali na nyumbani ugaibuni. Marekani, China, Ulaya wote wako mbioni kusoma
sheria na kaida zako ili wawe na nafasi katika karne hii ya utandawazi. Nimekuona
umepenya mpaka ndani ya technologia. Nina furaha kwa sababu niliyaona makao
yako kwenye mtandao. Bila shaka hutakufa kipenzi changu Kiswahili. Sasa kamusi
nyingi nimeziona zinazokuangazia wewe, na hata katika katiba ya Kenya wewe
ulijioatia nafasi yako madhubiti katika dola hili.
Afrika yote inakukumbatia tena kwa hamu. Kuna jambo
ambalo nimeliona ukilifanya lakini bado halijatimia. Sio lazima niwe nabii
lakini ninauwezo wa kusema hivi karibuni utakuwa wa kutumika Afrika nzima. Nimewaona
wakitafuta lugha moja ya kuwaunganisha
wana Afrika na alama zako ziko kidedea kuliko lugha za Fulani, Yoruba, Mande na Hausa ambazo zilipigiwa
kura kujitoza ulingoni kukabiliana nawe. Lakini linalo nipa tabasamu, ni kwamba
wewe bado uko mbali na wenzio kwa sababu ya historia yako ndefu na machapisho
kadha wa kadha. Pili usuli wako ni wa kibantu na lugha nyingi Afrika ni za
kibantu na ndio maana ikilinganishwa na wenzako, wewe una wasemaji wengi. Ndio maana
wasomi kama Wole Soyinka, Mohammed Hasan Abdulaziz na wengine walipokutana mjini Lagos Mwaka wa 1976, walikupigia kura na hakika hiyo siku itafika kipenzi changu
na utafikwa koja.
Ombi langu kuu kwako ni kwamba endelea kuzidi
kung`ang`ana na hatimaye utafanikiwa. Ndio najua una shida kidogo kidogo kama
za misamiati mingi tu ya kueleza mambo mengi ya kisayanzi na kiteknologia
lakini usife moyo kwani wenzako pia wamekopa. Hata wewe una uhuru wa kukopa.
Licha ya hayo watie wanao shime ili wasichoke katika utafiti kila siku na
kuleta misamiati kwa sababu wewe unakua kwa njia moja kubwa sana.
Nakuomba uzidi kuwakumbusha wale wanao eneza dhana
potovu kwamba wewe ni wa haiba ya chini ukiwapa mifano ya wanao wengi ambao
wameendelea sana kimaisha kupitia kukukumbatia
wewe. Nangoja kuona siku ile utatumika kama nembo ya kutambulisha Afrika
na dunia kwa jumla. Hakika hongera kipenzi changu kwa juhudi kubwa ulizonazo kwa kuwafaidi
wanadam na njia mufidi ya kuwasiliana. Mungu azidi kuwabariki wana na wapenzi
wako duniani.
Mwandishi: Franklin Momanyi. Mwanafunzi Chuo Kikuu cha Chuka.
Mwandishi: Franklin Momanyi. Mwanafunzi Chuo Kikuu cha Chuka.
Thursday, 23 October 2014
Mti unaobubujika maji katika kigogo chake
Mti mmoja katika mkoa wa Hamedan, magharibi mwa Iran umevutia watu wengi baada ya kububujika maji kwa wingi katika kigogo chake.
Wapita njia walivutiwa na mti huo, baadhi wamepiga picha, baadhi yao wamenawa nyuso, baadhi wamekinga maji hayo kwenye mifuko na vigeleni, alimradi umekuwa kivutio kwa watu mbalimbali.
kwa Hisani ya Iran Swahili Radio.
Subscribe to:
Posts (Atom)






