Friday 6 March 2015

Matatizo yanayokumba Kiswahili katika sajili ya mauzo/ biashara



Siku hizi za sasa, ni vigumu kuskiza redio bila kuyaskia matangazo ya  kibiashara. Unaposafiri njiani utakumbana na mabango makubwa makubwa yanayopasha wapita njia ujumbe fulani kuhusiana na bidhaa fulani. Kila kitu tunachotangamana nacho kwa njia moja au nyiingine, bila shaka huwa tunakumbana na matangazo ya kibiashara. Hata wakati mwingine tunapokea arafa za kutujulisha kuhusu bidhaa Fulani ama kutupa maelezo ya kutumia bidhaa Fulani. Lakini swali ni je, Kwa hizi njia zote ambazo zimetumika  ili kuwasilisha ujumbe, je lugha ya Kiswahili imetumiwa vipi katika nyanja hiyo? Je kwa njia yeyote ile, Kiswahili kimekuzwa? Na kama kimekuzwa ni kwa nini? Kama kimelemazwa, mbona, na nini kinachangia haswa hali hii?

Kabla ya kuenda mbali sana na makala haya, hebu tugusie  sajili ya biashara kwa sababu matangazo yote ya mauzo au kibiashara yapo katika sajili ya biashara.
·         Hutumia lugha ya chuku sana
·         Msamiati maalum
·         Kuchanganya ndimi
·         Matumizi ya picha na michoro
·         Matumizi ya nyimbo
·         Sentensi ndefundefu pale mteja anapoelezea mteja

Sifa za lugha inayostahili kutumika katika matangazo.
·          Nyepesi
·         Inayoweza fikisha ujumbe kwa mlengwa bila kujikanganya
·         Muktadha unaoeleweka (Context)
·         Inatumia jazanda  (Alex Grijelmo) anasema katika kitabu chake cha  "Seduction of the Words", kuwa matangazo ya mauzo yanatumia jazanda  - huru kama jua "Free as the Sun")
Kulingana na takwimu wakenya wengi  husoma kiingereza kuliko wale wanaopenda kusoma Kiswahili. Haswa hii ndiyo sababu moja ya matangazo mengi ya kibiashara kuwa yameandikwa kwa lugha ya kiingereza. Yakiandikwa kwa kiingereza ndio wanatafsiri ili kuwafikia wapenzi wa Kiswahili. Mara nyingi wakifanya utafsiri, kuna uwezo wa wao kupotoka na kutumia lugha ambayo si sanifu. Kwa mfano, Lipo tangazo linalosema ‘Triatix is for both small scale farmers and large scale farmers” linapotafsiriwa kuwa; Triatix ni ya wakulima  wadogowadogo na wakulima  wakubwa badala ya kusema, wakulima wenye mashamba madogomadogo na wale wenye mashamba makubwa makubwa.

Kiswahili kinanyanyaswa na kulemazwa sana na mahoka ambao mara nyingi hufikiria kwamba,  ili kuchekesha wakenya, lazima uvunje kaida za Kiswahili. Kwa mfano utasikia mahoka akiwa ulingoni akisema “Mtoto chake…..” Hii ni sawa?  Lakini tukumbuke kuwa wakenya wengi ndio wamesaidia kujenga hii taswira katika fikra zao. Naomba siku moja wakenya wagutuke na kuanza kuwa polisi wa lugha ya Kiswahili. Wakiona mtu akivunja sheria za kisarufi  basi moja kwa moja wamkosoe.

Tatizo lingine ambalo naweza sema kuwa linaleta shida ni watu kuwa na uzembe wa kutonunua kamusi ya kibiashara  na unchumi (TUKI) sababu ipo madukani. Na wakati mwingiine tukinunua, hatupati wakati wa kuiangalia. Kwa mfano matangazo mengi ya kibiashara huwa yanatumia neno “interest” badala ya riba, ama katika tangazo lile la Sona moja; kijana wa kimasai anasema “kichwa anauma” hii ni kuvunja sheria za kisarufi  kwa sababu kichwa kipo katika ngeli na KI-VI. Nashangaa angesema kichwa kinauma, ina maana hangeeleweka? Na watu wakiskia ile taasis wanayoiezi ikitumia jina la kiingereza kwa Kiswahili  ama kuvunja ngeli basi bila shaka nao hawatasita kufanya  vivyo hivyo. Na kwa kweli huwa hali hii inalemaza Kiswahili.

Changamoto nyingine ni kwamba baadhi ya misamiati inayotumika katika katika  mauzo haswa ya kitechnolojia haijapata kupatikana kwa Kiswahili. Kwa mfano; lile tangazo la faiba; “8bits per second” kwa kweli huwa ni vigumu kupata misamiati ya Kiswahili kuashiria hilo.

Wakati mwingine ni ukosefu wa uzoefu wa kutumia misamiati Fulani katika lugha ya mauzo. Lengo kuu la lugha ya mauzo ni kuhakikisha kwamba msikilizaji wa ujumbe ule ameweza kukunua bidhaa ama huduma inayotangazwa. Kwa sababu hii inawabidi kutumia lugha ambayo inaeleweka haraka na walengwa wa ujumbe ule. Kwa mfano; karo,kodi,rubuni, riba, kiinuamgongo ni aina ya malipo

Kulingana na takwimu, kuhesabu idadi ya watu nchini Kenya (2009),  wakenya wengi huskiliza Kiswahili mara nyingi   kuliko wale wanao skiliza redio za lugha ya kiingereza. Hii ina maana kwamba watu wengi huzungumza Kiswahili kwa sababu ki karibu na lugha zao za mama ambazo kwa aina Fulani zinakaribiana na kibantu. Swala hili linafanya redio zinazopererusha matangazo kwa lugha za Kiswahili kutangulia kwa idadi ya waskilizaji nchini. Kwa mfano, Citizen yaongozwa ikifwatiwa na radio jambo kisha redio maisha. Kisha stesheni  hizo zinapata mapato makubwa kutokana na mauzo ya jumbe za kibiashara. Kutokana na hii sababu, wanabiashara hujaribu kutumia Kiswahili ili kuwafikia wakenya wengi ambao huelewa Kiswahili kwa urahisi kuliko kiingereza ili kuongeza mauzo
mbalimbali.

Baadhi ya changamoto zinazokumba matumizi ya Kiswahili katika lugha ya mauzo/kibiashara.
1.       Ukosefu wa istlahi zilizo sawazishwa na kusanifishwa kutumika katika sajili ya biashara.
Kwa mfano
2.       Ukosefu wa uzoefu wa  kutumia kamusi za kibiashara (TUKI) kubaini maneno sahihi ya kutumia katika mustakabali mbalimbali.
3.       Ukosefu wa wa chombo maalum cha kuratibu shughuli nzima ya ukusanyanyaji, usanifishaji na hata usambazaji wa istalahi mpya za kibiashara katika vyombo vyote vya habari nchini
4.       Kwa sababu ya kutaka kueleweka kwa urahisi, wanabiashara hutumia lugha zingine mfano wa lugha ibuka kama SHENG ili kueleweka na hadhira ama walengwa wa ujumbe. Kwa mfano “shinda hao” na KCB
5.       Wale ambao wametwikwa jukumu la kutafsiri matangazo ya Kiswahili hawaelewi fika sheria, kaida na miiko inayoandamana na utumizi wa lugha ya Kiswahili.
6.       Ukosefu wa visawe au maneno yaliyo na maana sawa katika lugha asilia  na lugha pokezi kwa mfano bidhaa zinazohusiana na maswala ya kiteknolojia kama vile data bundles kwa matangazo ya bidhaa za mawasiliano.

Lakini si wakati wote ambapo Kiswahili kimelemazwa. Wapo wengine ambao ambao hukuza Lugha ya Kiswahili kwa mfano wale wanaoleta tangazo la sabuni ya ariel ambaopo wanasema madoa sugu badala ya madoadoa kama wengine husema.

Suluhisho la pekee kwa suala hili ni kurekebisha makosa hayo tumeangalia hapo awali ili tuweze kuwa na nafasi muhimu ya kuinua nafasi muhimu ya kukikuza Kiswahili chetu.
Kwa mfano; tubadilishe hii kasumba ya mahoka kuwa wakivunja kanuni za Kiswahili tusicheke,  na hilo litawabidi wabadirishe mbinu. itakuwa bora kusikia wa kenya wameanza kukitukuza Kiswahili na hili litawafanya wale wanaotunga jumbe za mauzo au  kibiashara kuzingatia sheria.
Pili wawe wakiajiri watu waliosomea taaluma  ya utafsiri kwa sababu makosa mengi tunayoyaona ni ni ya kutafsiri. Na kwa jumla kurekebisha Masuala ambayo tumeshayaguzia hapo awali…

Mtayarishi:  Frankline Momanyi
Chuo Kikuu cha Chuka.